UNE ni chombo cha utawala kinachoweza kulinganishwa na mahakama, ambacho hushughulikia malalamiko au rufaa za kukataliwa maombi au madai fulani na Idara ya Uhamiaji nchini (yaani UDI), kufuatana na Sheria Kuu ya Uhamiaji (yaani "utlendingsloven"). Kiutawala, UNE imewekwa chini ya Wizara ya haki (JD). Ijapokuwa Wizara inasimamia utawala wa UNE kwa kupitia sheria, kanuni, bajeti na aula za kijumla, lakini haiwezi kutoa mwongozo juu ya ufafanuzi wa sheria, utambuzi na ufahamu wa maamuzi, au maamuzi katika kesi fulani.
Daawa zinazoshughulikiwa katika UNE ni zile zinazohusu kimbilio la hifadhi ya kisiasa, kuja pamoja na kuunganika kwa familia iliyotawanyika, vile vile vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini, vibali vya uhamiaji na makazi nchini, kukataliwa ombi la kuwapo nchini, kufukuzwa nchini na maswala ya viza.
UNE ina waajiriwa mia mbili na hamsini, baina yao wakiwemo viongozi 27 wa Halmashauri ya dharura ya Rufaa, wenye elimu ya kimahakama. Pamoja na hao kuna wananchi 300 wasio weledi (yaani wananchi wasio wataalamu) ambao wamejitolea na kujishughulisha kama wanachama wa Halmashauri hiyo.
UNE ina njia zaidi ya moja ya kukata shauri au kufikia maamuzi. Maamuzi yanaweza kutolewa kwenye mkutano wa Halmashauri ya dharura ya Rufaa wakati mkata rufaa mwenyewe akiwa amehudhuria, hali kadhalika kwenye mkutano wa Halmashauri hiyo bila mkata rufaa kuhudhuria, yanaweza kutolewa na mwenyekiti wa Halmashauri peke yake au na ofisi ya usimamizi na urasimu (yaani "sekretariat") Mwenyekiti mmoja huamua utaratibu wa kuendesha kila daawa, na uamuzi kuhusu utaratibu uliochaguliwa hauwezi kulalamikiwa.
Kufuatana na Sheria Kuu ya Uhamiaji, daawa zisizo na shaka huweza kufanyiwa maamuzi yake bila ya mkutano wa Halmashauri ya dharura ya Rufaa, na hufanyiwa maamuzi hayo na mwenyekiti peke yake au na ofisi ya usimamizi na urasimu. Hizi huwa miongoni mwa daawa zile ambazo zinaambatanika kwa urahisi kikanuni, ambapo huwa rahisi kuthibitisha kama matakwa au masharti maalumu katika sheria na kanuni yametimizwa. Ni hasa zile daawa ambazo zinakuwa na shaka dhahiri ambazo hupelekwa mbele ya Halmashauri ya dharura ya Rufaa.
Mikutano mingi ya Halmashauri ya dharura ya Rufaa huitishwa wakati mkata rufaa mwenyewe akihudhuria. Lakini vile vile mikutano mingine hutendeka bila mkata rufaa mwenyewe kuwepo. Kwa mfano ikiwa mkata rufaa na Idara ya Uhamiaji nchini wamekubaliana juu ya uhakika fulani wa kimsingi kuhusu daawa fulani, yaani maelezo ya mkata rufaa yametiwa maanani wakati daawa ilipopelekwa UNE, basi mkutano wa Halmashauri ya dharura ya Rufaa unaweza kuitishwa bila mkata rufaa kuhudhuria. Kwa upande mwingine kuhudhuria kwa mkata rufaa ni muhimu pale ambapo kuwepo kwake kunachangia katika kufafanua uhakika fulani katika kesi.
Kwenye mikutano ya Halmashauri ya dharura ya Rufaa hushiriki mwenyekiti mmoja wa Halmashauri pamoja na wanachama wawili wa Halmashauri wasio weledi (yaani wananchi wasio wataalamu). Ofisi ya usimamizi na urasimu ya UNE ina jukumu la kutayarisha daawa ambazo zitashughulikiwa kwenye mkutano wa Halmashauri ya dharura ya Rufaa. Mwenyekiti wa Halmashauri ya dharura ya Rufaa huwasilisha nyaraka za daawa kwa wanachama watakaoshiriki kwenye mkutano kabla ya mkutano huo. Mikutano kama hii hufanyika faraghani.
Halmashauri ya dharura ya Rufaa hufunguliwa kwa kutolewa muhtasari wa daawa, maelezo ya matakwa na masharti yanayohusika katika Sheria Kuu ya Uhamiaji na kanuni za uhamiaji nchini, pamoja na maelezo juu ya maswala ya maana na umuhimu katika daawa. Katika daawa ambapo mkata rufaa anahudhuria, mkata rufaa hupewa nafasi ya kutoa maelezo ya habari na tathmini zenye maana katika daawa hiyo. Wanachama wanapewa nafasi ya kumhoji mkata rufaa. Wakili au mwakilishi wa kisheria wa mkata rufaa anapewa nafasi ya kutoa muhtasari wa daawa. Daawa ambazo hushughulikiwa katika mikutano ya Halmashauri ya dharura ya Rufaa hutolewa maamuzi yake kwa wingi wa kura (yaani kwa kupigiwa kura).
Maamuzi yanayotolewa katika daawa mbalimbali, hayawezi kupitiwa upya na wizara, serikali au na uongozi wa UNE.